Atwoli: Wakati wetu tukiwa Azimio kumfikia Uhuru ilikuwa ngumu, wala hakufanya mengi

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Francis Atwoli, sasa anadai ilikuwa vigumu kumfikia Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, akidai kwamba mara nyingi alisita kushirikiana na mawaziri na viongozi wa kisiasa kuhusu masuala muhimu ya kitaifa.

Akizungumza Khwisero, Kaunti ya Kakamega, jana Bw Atwoli alisema Bw Kenyatta alikuwa mgumu kufikiwa ikilinganishwa na marais wengine aliowahi kufanya nao kazi.

“Nimefanya kazi na marais wote na namjua Uhuru Kenyatta. Kama si juhudi za Naibu Rais wa wakati huo William Ruto, hata kuwafanya wabunge wakutane na Rais haikuwa rahisi,” akasema.

Kauli hii inajiri wakati uhusiano kati ya Bw Kenyatta na Rais Ruto ukiwa na mashaka. Mnamo Disemba 9, 2024, Rais Ruto alimtembelea Bw Kenyatta nyumbani kwake Ichaweri, Gatundu, katika juhudi za kurejesha uhusiano wao baada ya miaka kadhaa ya tofauti kali za kisiasa.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na Taifa LeoRais Ruto alisema pia alikuwa amemtembelea Kenyatta katika afisi yake karibu na Ikulu ili kumshawishi kuunga mkono ajenda ya kitaifa.

“Nilienda kumuona Ichaweri na pia katika afisi yake iliyo hapa karibu (na Ikulu) na nikajaribu kumshawishi kwamba kama kiongozi wa zamani wa nchi, na ndiye pekee aliye hai sasa, ilikuwa bora atusaidie kujenga nchi, lakini alisita. Hakuwa na uhakika kama alitaka kufanya hivyo na hayo ni maamuzi ambayo watu hufanya. Alichagua kushirikiana na upinzani, akiwafadhili,” akasema Rais.

Rais Ruto alisema wazo la viongozi hao kushirikiana lilitokana na mazungumzo yake na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, aliyefariki Oktoba 2025.

“Sasa sisi ndio wazee. Sisi ndio viongozi wa taifa hili. Kwa nini tusishirikiane, tujenge taifa ambalo tunaweza kulikabidhi kwa kizazi kijacho cha viongozi?” akasema Rais Ruto.

Bw Atwoli pia aliwaonya wakazi wa Magharibi dhidi ya kugawanywa kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, akionekana kumlenga Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna.

“Jamii ya Waluhya ni rahisi kudanganywa lakini nataka muwe macho,” alisema.

Alisema pia urais hauwezi kupatikana kupitia michango midogo ya wananchi.

“Njia ya kuelekea urais si rahisi. Huwezi kutembea na ndoo sokoni ukikusanya Sh50 kutoka kwa mama mboga. Hizo haziwezi kukufanya uwe rais,” akaongeza.

Bw Atwoli pia alimtaka Bw Kenyatta kumruhusu Rais Ruto kukamilisha muhula wake bila kuingiliwa.

“Tayari alihudumu mihula yake miwili bila chochote cha maana cha kuonyesha. Kwa nini sasa asikae chini na kumruhusu Rais Ruto kuwahudumia Wakenya?” akauliza.

Kiongozi huyo wa COTU pia alimkosoa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale kwa kugeuza mazishi ya mkewe marehemu, Gloria Khalwale, kuwa jukwaa la kisiasa.

 

 

Na DOMNIC OMBOK

More From Author

How Canada could hit back to hurt the US economy – and Trump

Ayacko: Hatutaki viongozi wa Linda Mwananchi Migori

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *